Watu wengi wanashindwa kuendesha biashara zao vizuri. Kwa sababu mara nyingi wao huangalia vitu juujuu tu, au huamua kuiga vya watu. Wengine huwaza sana kuhusu ndoto zao za mafanikio kuliko nini kinaendelea katika biashara yao. Kuwa na ndoto kubwa ni muhimu na mimi ni mmoja wa watu wanaoamini katika kuwa na ndoto ili kujisukuma ufanikiwe. Napenda kufikiria siku ambayo nitamiliki Manchester United. Ni moja kati ya ndoto zangu kubwa kabisa. Lakini tatizo linakuja pale wafanyabiashara wanaposahau upande wa kufanya kazi kwa juhudi hata katika kazi usizozipenda. Vitu kama kuzunguka ukifanya utafiti wa soko, kufanya kazi kwa muda mrefu pamoja na changamoto zozote utazokutana nazo katika safari kuelekea mafanikio.
Utaona hili kwa wafanyabiashara wengi ambao wanategemea mbinu walizotumia miaka mitano iliyopita zikaleta mauzo makubwa basi mbinu hizohizo zilete mauzo makubwa leo hii. Watu wanakuwa wavivu kujifunza teknolojia mpya zinazotoka na jinsi zinavyoweza kuwasaidia kukuza biashara zao. Hawaelewi kuwa mambo yamebadilika na mafanikio yako ya kesho yatatokana na jinsi unavyojiboresha kutokana na mabadiliko yanayotokea leo. Uchapakazi pamoja na ujuzi vinajengwa kutokana na juhudi katika kufanya kazi zote ndani ya biashara yako kwa bidii.
Kama huweki juhudi katika kuwa bora zaidi basi kadri siku zinavyoenda utapotea sokoni. Nenda kawaulize Nokia na kiwanda cha Bora Shoes watakupa ushahidi. Unahitaji kuweka juhudi kila siku au utashindwa. Mfano mzuri ni wakati Facebook imeanza kupanda chati nchini Tanzania mwaka 2011. Kilichokuwa kinanishangaza ni jinsi biashara zilivyokuwa zinadharau uwezo wa Facebook katika kuwaongezea mauzo. Na kwa ambao walikuwa wanafahamu kinachoendelea kulikuwa na fursa kubwa. Niliingia ubia na moja ya makampuni jijini Dar nikawa nawauzia bidhaa zao katika ukurasa wa Facebook kwa kutumia jina lao. Makubaliano yalikuwa nikipata oda Facebook naenda kuchukua bidhaa kwao BURE napeleka kwa wateja na kuuza kwa bei ya juu zaidi kisha nawalipa hiyo kampuni bei karibu na jumla. Ni moja kati ya madili mazuri niliyowahi kupata kwani ndani ya miezi 3 nilishaingiza faida ya zaidi ya milioni moja nikiwa nafanya kazi masaa machache sana. Nikiwa na miaka 16 tu, hizo zilikuwa hela nyingi sana. Kama hiyo biashara ingetambua nguvu ya Facebook basi faida yote hiyo ingekuwa yao. Leo hii naona hikihiki kinatokea katika Snapchat. Nishaanza kutafuta dili lingine.
Napenda kusisitiza kuwa ili uwe mfanyabiashara mkubwa inabidi uweke juhudi katika kila kazi inayohusiana na biashara yako hata zile usizopenda. Usipofanya hivyo wenzako watakuacha nyuma ukila vumbi lao. Ukiona teknolojia mpya inakua, jifunze jinsi ya kuitumia kukuza biashara yako. Mara kadhaa inaweza kuhitaji hata miaka kujifunza ili upate matokeo unayotaka, ila hili lisikukatishe tamaa. Ukweli ni kwamba unafanikiwa kwa kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii. Piga kazi ufikie ndoto zako.
Una ndoto gani unataka uifikie? Nieleze hapo chini katika comments.
Kuwa na ndoto ni hatua ya kwanza kuelekea mafanikio. Hatua inayofuata ni kuweka mipango jinsi ya kuzifikia.
Imeandikwa na SIMON MNYELE

ConversionConversion EmoticonEmoticon