adsense

KUSAIDIA NI NEEMA



Miaka 40 iliyopita, Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Kikatiba nchini Afrika Kusini, Raymond Zondo, alikuwa kijana maskini lakini aliyefaulu vizuri kwenda kusoma shahada ya kwanza ya sheria.
Alipata ufadhili wa Serikali, kwa hiyo suala la yeye kusoma halikuwa na pingamizi. Tatizo likawa anaiachaje familia yake? Mama yake hakuwa na uwezo wa kutengeneza kipato kwa ajili ya familia. Mama yake alikuwa analea ndugu zake wengine tegemezi.
Zondo aliwaza: "Naiachaje familia? Itaishije bila kipato wakati wote nikiwa masomoni?" Hayo ndiyo maswali yaliyomtesa Zondo.
Wanasema penye nia kuna njia. Zondo baada ya kutafakari sana, aliamua kumfuata mfanyabiashara mwenye asili ya Bara la Asia, Sulaiman Bux, wa maduka ya Moosa Bux Bazaar, yaliyopo Ixopo, KwaZulu-Natal, Afrika Kusini.
                                                       

Zondo alipokutana na Bux, alimuomba amkopeshe fedha za chakula ili amwachie mama yake kipindi chote akiwa masomoni na angemrejeshea baada ya kumaliza shahada yake.
Bux alikubali kumkopesha Zondo, lakini akakataa kumpa fedha taslimu. Bux aliahidi kumpa mama yake Zondo vinywaji vyenye thamani ya Randi 40 (Sh7,080) kila mwezi. Vinywaji hivyo mama yake Zondo aliuza na kupata fedha za chakula. Zondo anasema kuwa fedha hizo zilikuwa nyingi wakati huo na zilitosha chakula kila mwezi.

Miaka mitatu baadaye, Zondo akiwa amehitimu shahada yake ya sheria, alimfuata Bux na kumwomba utaratibu wa kumlipa fedha alizomkopesha kwa miaka mitatu akiwa masomoni kwa ajili ya chakula cha mama yake na familia.
Bux alimjibu Zondo: "Nenda kawatendee wengine kama ambavyo nimekutendea." Kimsingi Bux hakutaka malipo kutoka kwa Zondo.
Leo hii Zondo ni Naibu Jaji Mkuu wa Afrika Kusini. Bux alimsaidia kipindi kigumu bila kujua kuwa aliyemsaidia angekuja kuwa mtu muhimu kwenye nchi.
Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mogoeng Mogoeng, alimtaka Zondo aelezee historia yake ya kusaidiwa na Bux kwa sababu Afrika Kusini kuna maskini wengi ambao wanaweza kuhamasika kutokana na historia yake. Video ya Zondo akielezea jinsi alivyosaidiwa na Bux imevutia mamilioni ya watu duniani.
Bux alipoulizwa na Radio Islam ya Afrika Kusini, alisema hakutarajia kupata shukurani kutoka kwa Zondo, ila akasema ni utaratibu aliojiwekea wa kusaidia wenye uhitaji pasipo kutarajia malipo kwa sababu huo ndiyo utaratibu wa Kiislamu.

POKEA HII

Ukimsaidia mwenzio unaingia kwenye historia yake. Bux yumo ndani ya historia ya Zondo.
Usipomsaidia mwenzio haimaanishi hatafika alikopangiwa kufika, Mungu anayetaka afike, atamfikisha kupitia kwa mwingine ambaye ataingia kwenye historia yake. Wewe utakosa fursa ya kuingia kwenye historia hiyo.
Soma Hebrania 6:10: Mungu si dhalimu hata asahau kazi yenu na upendo mliomwonyesha mlipowasaidia watu wake na mnavyoendelea kuwasaidia.
Kumbe sasa unavyosaidia watu wengine, hufanyi kwa ajili yao, bali msaada kwa wengine ni upendo kwa Mungu.

imeandikwa na: Luqman MALOTO
Previous
Next Post »