adsense

Hili Ndilo Kusudi La Maisha Yako Hapa Duniani.



Karibu katika mtandao wa Inuka Mtanzania, mtandao mahsusi kwa ajili ya kukupeleka kileleni mwa mafanikio. Leo katika makala yetu, naomba nikumegee maarifa muhimu yatakayo kufunulia kusudi la maisha yako. Maana watu wengi sana wanaangaika kujua kusudi la maisha yao hapa duniani lakini hawafanikiwi kujua; hivyo kupitia maarifa utakayoyapata kutoka katika makala hii, nina uhakika hayatokuacha kama ulivyokuwa.

Kusudi la maisha yako ni tatizo au changamoto uliyozaliwa kuitatua; yaani kwa maneno mengine ni kwamba, wewe umeumbwa kuwa mtatuzi wa tatizo fulani hapa dunia. Umeumbwa kwa ajili ya kitu fulani ambacho ni wewe tu unayeweza kukifanya kwa ubora huu; na kupitia kusudi hilo ndipo maisha yako yanaweza kupata maana. Kupitia  Kusudi la maisha, ndipo tunaweza kupata kipimo cha mafanikio, yaani ni kwamba, tafsiri ya kufanikiwa au kutokufanikiwa inapata maana kwa kuzingatia utekelezaji wa kusudi.
Unaposimama kwenye kususdi lako ndipo unaweza kuelezea kiwango cha mafanikio ulichofanikisha. Kwa hiyo ni kusema, mafanikio si kuwa na fedha, umaarufu, umiliki wa mali, au kuwa na afya, bali mafanikio ni kiwango cha ufanikishaji kusudi la maisha yako. Hivyo mafanikio hayapimwi kwa kujilinganisha na wengine, bali yanapimwa kwa kulinganisha ulichokifanya au kukifikia kwa kuzingatia kusudi ulilobeba.


Sasa unawezaje kugundua kusudi la maisha yako? Kujua kusudi la maisha yako, ni kwa kujichunguza na kujitathimini wewe mwenyewe. Angalia ni kitu gani unachokipenda au unashauku kubwa nacho, yaani angalia ni kitu gani ambacho ukikiona kinaenda tofauti na kinavyopaswa kuwa kinakuumiza sana? au unaweza kuangalia nini tamanio lako la kuleta neema, yaani, ni eneo gani la maisha ambalo unatamani kusaidia ili liende juu au liwe bora kuliko awali? kupitia hayo maswali hakika waweza kujua kusudi la maisha yako.

Mfano, kusudi lako linaweza kuwa ni udaktari wa binadamu, kutokana na kutamani kutibu watu, au unaweza kuwa wewe ni mwalimu, kwa sababu ya tabia yako ya kupenda kufundisha wengine. Au yaweza kuwa wewe ni mwanamuziki, kutokana na tabia yako ya kupenda muziki na kujisikia kuimba. Yote hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo yanaweza kukusaidia kugundua kusudi la maisha yako. Kwa upande wangu, mimi nilikuwa napenda kuona watu wanapata maarifa, hivyo nikagundua kusudi la maisha yangu.



Kadhalika unaweza kugundua kusudi la maisha yako kupitia maono uliyonayo, maana maono ni ufunuo wa kusudi la maisha yako kupitia picha. Mimi nilikuwa na maono ya kuwa mbele ya watu nikitoa mafundisho, maono ambayo nilikuwa nayo kwa muda mrefu sana lakini baada ya kuchunguza kwa kina nikagundua ndilo lilikuwa ni kusudi langu; hivyo basi nikaanza kusimama kutokea hapo, na kila siku naendelea kusonga mbele.
Kumbuka usipofahamu kusudi la kitu utakitumia vibaya, vivyo hivyo usipojua kusudi la maisha yako bila shaka utatumia nguvu, akili na uwezo wako vibaya hasa katika vitu ambavyo si vya msingi. Na ukijitumia katika vitu ambavyo hukuumbwa kuvifanya, iwe unaiga au unajilazimisha kufanya, ni ngumu kuwa na maisha ya furaha au utoshelevu; maana furaha na utoshelevu ni zao la kusimama kwenye kusudi lako.


Mwisho, ni vyema utambue kuwa, jukumu la kugundua kusudi la maisha yako ni lako wewe na si la mwingine, sisi wengine twaweza kukuongoza tu kugundua lakini si kukueleza kuwa wewe umeumbwa kufanya nini maana jibu unalo wewe. Hivyo endelea kujitathimini mpaka ugundue kitu ambacho ukikifanya unajisikia furaha isiyo kifani.

Nategemea kwa hayo tuliyojifunza hapo juu yatakusaidia kugundua kusudi la maisha yako, kama utashindwa usikate tamaa endelea kusoma makala zetu kila siku na siku si nyingi utagundua tu. Asante kwa kuongozana nami hadi tamati, endelea kusoma makala zetu zaidi katika mtandao huu.
Previous
Next Post »