adsense

Ili Ufikie Uhuru Wa Kifedha (Utajiri) Inakupasa Kugawa Mshahara, au Kipato Chako Katika Maeneo Haya.

             Image result for divided

Rafiki yangu na msomoji wa mtandao wa Inuka Mtanzania, habari yako? Natumaini unaendelea vyema na shughuli zako; hongera sana, na endelea kutia bidii katika hicho ulichokichagua kukifanya, maana bidii ni tunda la watu wenye imani juu ya kile wanachokifanya. Maana imani ni kuchukua hatua ya kile unachokiona kwa picha katika akili yako.

Leo katika makala yetu, nitakwenda kukuangazia maarifa muhimu kuhusu fedha. Maana ni ukweli usiopingika kuwa watu wengi hawana elimu hii katika maisha, lakini kama ilivyo jukumu letu kupitia mtandao huu, napenda kukuhakikishia kuwa tutakuelimisha vya kutosha katika eneo hii la maisha ya mwanadamu. Hivyo changamoto kama madeni, matumizi holela ya fedha na mengineyo kuhusu fedha hayatakuwa ni mtihani tena katika maisha yako.


Leo katika makala hii, nitakuelekeza  kwa undani kabisa kuhusu mgawanyo wa fedha unayotengeneza au mshahara unaoupata, ikiwa ni muendelezo wa elimu ya fedha. Lengo likiwa ni kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha (utajiri) kama yalivyo matamanio yako. Ni ngumu sana kufikia hatua hii ya uhuru wa kifedha kama hutajua misingi ambayo unapaswa kuisimamia.



Eneo la Kwanza, Matumizi. Mshahara au kipato, kwanza kabisa kinapaswa kuelekezwa kwenye matumizi yako ya kila siku. Matumizi ya kila siku kimsingi yanahitaji fedha ili kuyafanikisha, hivyo kutoka kwenye mshahara wako ni lazima uyatengee fedha kwa ajili ya kuyahudumia. Hapa ninamaanisha utenge fedha kwa ajili ya chakula, mavazi (hasa yanapohitajika), mahitaji ya familia, usafiri, ankara, matibabu, dharura nakadhalika.



Katika hili eneo, kumbuka unapaswa kuwa makini sana hasa kwa kuelekeza fedha katika vitu vile ambavyo ni vya muhimu; na kuepukana kabisa na vile ambavyo si vya muhimu au si saizi yako. Usipende kufanya matumizi kwa kuiga wengine au kukuza haiba yako zaidi ya ulivyo. Ishi maisha ya uhalisia wako kabisa.

Eneo la pili, Akiba. Hili ndilo eneo ambalo ni chanzo cha uhuru wa kifedha katika siku zako za usoni. Unapaswa kuweka akiba kutoka kwenye kila kipato chako, na hili halina mjadala, ni jambo muhimu sana unalopaswa kulianza na kuliishi. Ukiona unashindwa kuweka akiba kutoka kwenye kipato unachokitengeneza, basi ujue wewe ni mpumbavu kama Biblia inavyosema; yaani mishipa yako ya hekima itakuwa inamepasuka. Biblia inasema “......mpumbavu huponda mali yake yote” Mithali 21:20.



Kwa hivyo acha visingizio, weka akiba. Ukishindwa kuweka akiba katika kipato ulichonacho sasa, basi ujue hata kiongezeke pia utashindwa kwa sababu kuweka akiba ni tabia na tabia hujengwa. Akiba ndiyo chanzo cha uwekezaji.

Eneo la tatu, UWekezaji. Eneo la mwisho ambalo unapaswa kuligawia kipato chako ni eneo hili la uwekezaji. Uwekezaji ndiyo njia pekee inayoweza kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha au utajiri. Lakini kama nilivyosema uwekezaji unaenda sambamba na kiwango cha akiba unachokiweka kila siku au mwezi. Kwa hiyo unapokuwa na akiba hatua ya pili unayoichukua ni kuiwekeza akiba hiyo.

Kwa hiyo weka akiba kwa kipindi fulani kulingana na kiasi cha fedha unachokihitaji, kisha iwekeze. Maeneo ambayo naweza kukushauri kuwekeza fedha yako ni kwenye ununuzi wa hisa, amana, hatifungani au kwenye mfuko wa vipande (UTT). Uwekezaji katika maeneo haya unawezekana kwa sababu unahitaji mtaji kidogo sana ili kuwekeza, na pia eneo hili ni zuri kwa wale ambao wanataka kuhifadhi ela ya kwa muda mrefu kabla ya kuipeleka katika uwekezaji Mwingine; maana kuliko kuhifadhi fedha yako benki au kwenye kibubu bila kupata faidia yoyote, unaiweka katika maeneo hayo ili iweze kuongezeka.



 Pia unaweza kuwekeza katika biashara ya moja kwa moja au katika majengo na aridhi kulingana na kiwango cha akiba ulichonacho. Eneo hili linahusu zaidi watu wenye akiba kubwa tayari. Kumbuka kuwekeza ni sawa na kutengeneza mfereji wa fedha utakaotiririsha maji upande wako siku za usoni.

Hayo ndiyo maeneo matatu makubwa unayopaswa kuelekeza kipato au mshahara wako ili kujihakikishia uhuru wa kifedha au utajiri katika siku za usoni. Maeneo hayo ni lazima uyagawie fedha, kinyume chake utaishi maisha magumu sana pale nguvu, au uwezo wako wa kufanya kazi utakapopungua. Ni vyema kutambua kuwa maisha hayatabakia kama yalivyo sasa.
Previous
Next Post »