adsense

Watu hawanunui kile unacho uza bali watu hununua ubunifu wa kile unacho kiuza!.


Image may contain: text

Habari yako ndugu yangu, karibu katika makala ya leo, makala muhimu kwa ajili ya kukupandisha kileleni mwa mafanikio yako. Kila siku ipitayo ni muhimu, usiipuuze na kuruhusu ipite bila ya wewe kutenda chochote ambacho ni muhimu katika maisha yako. Vitu muhimu katika maisha yako ni vile vyote ambavyo ni vipaumbele vya maisha yako, vile vinavyokupeleka kule unakotaka kupafikia.

Rafiki yangu, leo nitakwenda kukuonyesha nguvu ya kung’ang’ania kufanya kile ulichochagua kukifanya. Katika maisha huwezi kufikia mafanikio yoyote yale kama hutaongeza thamani yako, thamani uliyonayo ndiyo hubadilishwa na fedha unazozihitaji. Fedha ni kisaidizi tu kinachotuwezesha kuhifadhi na kubadilishana thamani. Fedha haihitajiki kama livyo kwa matumizi. Huwezi kula fedha, huwezi kulalia fedha,  unahitaji kula chakula na kulalia kitanda ambavyo vinapatikana kwa fedha.


Thamani yoyote unayoweza kuongeza katika maisha ya wengine iwe kwa kupitia kazi au biashara unayofanya, ndiyo inayolipiwa. Unalipwa fedha baada ya kutatua matatizo au changamoto za watu. Kwa kutatua changamoto hizo ndipo unapolipwa fedha kulingana na kiasi cha thamani ulichowaongezea wengine. Kwa hiyo kiasi cha fedha ulichopokea huendana na kiasi cha thamani ulichokitoa. Ikitokea na wewe una changamoto inayohitajika kutatuliwa, ina maana na wewe unahitaji kulipia kiasi cha fedha kinachoendana na kiwango cha thamani unachokihitaji katika kutatuliwa tatizo lako. Kwa hiyo unaweza kuona fedha ni mchezo wa mabadilishano ya thamani.


Kwa hiyo ni kusema bila kuwa na thamani ambayo utaiongeza kwenye maisha ya watu huwezi kuwa na fedha, labda uibe, na uibe kila siku, maana hutaweza kuzivuta fedha kihalala. Ili uweze kuongeza thamani katika maisha yako ni lazima ubobee, kubobea ni kule kuwa bora au kiongozi katika eneo fulani la maisha. Huwezi kufanya kila kitu, ila unaweza kuwa wakawaida kama utafanya vitu zaidi ya kimoja; lakini ubobezi katika maisha huja pale uchaguapo eneo moja la maisha ambalo utalishughulikia. Kubobea ni matokeo ya kuchagua kuwa bora katika eneo fulani la maisha.

Kama unataka kuendelea kuwa na maisha ya wastani maishani mwako, endelea kufanya mambo mengi au kufanya jambo moja lakini si kwa ubora. Maisha ya wastani ni  yale maisha ambayo huna fedha za kutosha kutimiza mahitaji yote uliyonayo. Watu wote ambao wamefanikiwa sana katika maisha yao ni wale ambao walitumia rasilimali nguvu, akili na muda wao katika eneo moja la maisha.


Chagua eneo moja muhimu katika maisha yako, kusudi lako, wekeza huko muda, akili, na nguvu zako zote ili ubobee katika eneo hilo. Ng’ang’ania hicho ambacho umechagua kukifanya. Kifanye kila siku, kifanye kuwa ndicho kipaumbele chako kikuu. Kifanye tena na tena, hata ikitokea huoni matokeo yoyote ya kudhiridhisha mwanzoni, wewe kifanye tena na tena na tena. Watakuja watu wenye maneno mabaya watakucheka, watakuona kama umechanganyikiwa au hujielewi, wewe ng’ang’ana bila kuacha. Kadiri utakavyokuwa unang’ang’ana nacho ndivyo kadiri utakavyokuwa unayakaribia mafanikio yako, na kasi yako ndipo itakavyoongezeka zaidi.

Asante kwa kuongozana nami toka mwanzo hadi tamati; endelea kujifunza kupitia mtandao huu kila siku bila kusahau kuwaalika na wengine kujifunza nasi.

Author; Alex mushi.
Previous
Next Post »