Alex Mushi May 22, 2017
Habari yako rafiki yangu, natumaini unaendelea vyema na shughuli za kuyaboresha maisha yako. Hii ni siku nyingine ambayo Mwenyezi Mungu kakujalilia, hakika ni siku bora na nzuri kwa ajili ya kuendelea kutimiza yale uliyoyachagua kuyafanya. Karibu katika ukurasa wa siri ya mafanikio, ukurasa mahsusi kwa ajili ya kukufunulia siri muhimu katika safari ya mafanikio.
Katika ukurasa huu leo, nitakwenda kukushirikisha, mtu hatari na sumu wa biashara yako. Ki msingi kila biashara huazishwa kwa lengo la kuingiza kipato, na kila mwenye biashara hutamani sana biashara yake kukua na hatimaye kumfikisha katika uhuru wa kifedha. Lakini, wengi wamekwama kufikia matarajio hayo, kiasi cha kupelekea, kuamini biashara ni ngumu na wanaoweza kuzifanikisha, ni wale tu ambao wana bahati.
Lakini, ni hivi, Si kweli kwamba wenye bahati ndiyo wanaoweza kuzifanikisha biashara zao, bali mtu yeyote anaweza kufanikisha biashara yoyote anayoifanya kama atafahamu siri hii. Kuwa mtu hatari na sumu wa biashara yake, ni mteja asiyeridhika. Mtu huyu huzuia biashara nyingi sana kukuwa na kuzifanya zidumaye. Na mara nyingine huziua kabisa biashara husika.
Mteja asiyeridhika na huduma au bidhaa yako, mara nyingi yeye ndiye hugeuka kuwa adui wa biashara yako kwa wateja wengine. Unapotoa huduma isiyoridhisha na mteja akaondoka na manung’uniko, manung’uniko yale huwa hayaishii kwake tu, bali huyasambaza kwa wengine, na wengine huyasambaza kwa wengine; na kama utakuwa ulitoa huduma isiyoridhisha kwa wateja zaidi ya mmoja basi kuwa na hakika athari ya manung’uniko yao yatasambaa zaidi.
Epuka sana kutoa lugha mbovu, dharau, lugha ya kibabe, huduma isiyo na kiwango au kumdanganya mteja katika biashara yako, maana kufanya hivyo ndiko hupelekea mteja kutokuridhika na kuondoka na manung’uniko. Katika dhama za sasa, ambako biashara zinaushindani mkubwa ni lazima ujifunze kutoa huduma bora na yenye thamani kubwa kwa wateja wako. Ukikosea kwenye hilo kuwa na hakika wateja watakukimbia.
Huduma bora kwa mteja hata kama ni mmoja inatosha kuwavuta wateja wengi zaidi, kwa sababu, kama ambavyo ubaya wa huduma yako husambaa, ndivyo hivyo hivyo uzuri wa biashara yako husambaa kwa wengine na kukuvutia wateja zaidi. Jifunze kutoa huduma bora na yakuridhisha kwa mteja wako, yaani mthamini hata kama ni mmoja. Tumia lugha nzuri, kuwa mkweli kwake, na pia kuwa muungwana kwake hata kama kuna tatizo lilitokea kimakosa ambalo lilikuwa juu ya uwezo wenu.
Kwa hiyo ukitaka kufanya mageuzi makubwa katika biashara yako, anza kumjali mteja wako. Asante kwa kuongozana nami toka mwanzo hadi tamati.
ConversionConversion EmoticonEmoticon